Matangazo:

kutangaza biashara yako hapa piga simu 0718865251 au email: excitetanzania.gmail.com

HABARI KAMILI

Tuesday, December 24, 2013

YANGA KUMLIPA BRANDTS MILIONI 170 KWA KUVUNJA MKATABA

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Ernie Brandts sasa atavuna Sh170 milioni kutoka kwa uongozi wa timu hiyo baada ya kusitisha mkataba wake jana.
Kutokana na hali hiyo, Yanga italazimika kumlipa mshahara wake wa miezi 10 iliyobakia ambayo ni zaidi ya Sh170 milioni kwa kuwa kocha huyo alikuwa akilipwa mshahara wa Dola 10,000 kwa mwezi.
Uamuzi wa kumtimua kocha Brandts umefikiwa kwenye kikao cha kamati ya utendaji ya Yanga iliyoketi juzi Jumamosi muda mchache baada ya timu hiyo kunyukwa kwa mabao 3-1 na watani zao Simba katika mchezo wa Nani Mtani Jembe.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo iliyopo mtaa wa Twiga na Jangwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Abdallah Bin kleb alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maoni ya wachezaji mbalimbali wa zamani kuhusu kiwango cha timu.
“Tumempa notisi ya siku 30 ili tuendelee kutafuta kocha mwingine na tupo kwenye mchakato wa kumlipa stahiki zake, tuachane kwa amani.
“Mwanzoni alipandisha kiwango cha timu, kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye kwa sababu hana jipya, sisi tunalenga michuano ya kimataifa zaidi sasa kwa kiwango hiki hatutafika mbali ni lazima tuchukue hatua za haraka zaidi,” alisema.
Kuhusu wajumbe wengine wa benchi la Ufundi, Bin Kleb alisema kwamba taratibu nyingine zinafuata na ndani ya wiki hii kuna matukio mengi makubwa ambayo klabu yake itayafanya.
Hata hivyo tayari Brandts alikabidhiwa barua yake ya kusitishiwa mkataba rasmi juzi na jana baada ya mazoezi Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga alikutana na wachezaji na kuzungumza nao kwa zaidi ya nusu saa.
Naye Brandts alipozungumza na gazeti hili kuhusiana na kuvunjiwa mkataba alisema kwa kifupi “Nasubiri notisi ya siku 30 imalizike, kuna kitu nitaongea, lakini sasa hivi msikilizeni Abdallah (Binkleb) anachosema ukifika muda na mimi nitazungumza.”
Yanga imevunja mkataba na kocha huyo ukiwa umepita mwezi mmoja tangu wamwongezee mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa timu hiyo.
Licha ya kufungashiwa virago, kocha, Brandts ameonyesha kukasirishwa na nidhamu mbovu ya mastaa wake.
Kwenye mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Bora Kijitonyama, nyota wengi wa klabu hiyo hawakufika mazoezi bila ya kutokuwa na taarifa zao zaidi ya Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye amefiwa na bibi yake.
Baadhi ya wachezaji ambao walikacha mazoezi ya kocha huyo ni Ally Mustapha, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza.
“Sielewi, walitakiwa leo wawepo mazoezini, lakini sijawaona, sina taarifa zao labda ni kwa vile maprofesheno, sielewi.
“Profesheno nidhamu ni kitu cha kwanza, lakini hapa profesheno ni tofauti anaamua vile anataka, najua Chuji amefiwa na bibi yake, lakini Okwi na wenzake sielewi chochote labda viongozi wanajua walipo mimi sijui.”
Yanga itaondoka Januari 2 kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi na Januari 14 itakwea pipa kwenda Hispania kwa kambi ya siku 10.
Share it Please

Excite Media

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.

0 comments:

Post a Comment

Copyright @ 2013 SHAUKU BLOG. Designed by Templateism | Love for The Globe Press