Dodoma/Dar es Salaam. Baadhi ya wabunge
wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
katika kile wanachodai kuwa hawaridhishwi na utendaji wake serikalini.
Hiyo ni dalili kwamba kung’oka kwa mawaziri wanne
kutokana na matokeo ya ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili hakujamnusuru Pinda, kwani baadhi ya wabunge wanaendelea na
msimamo kwamba naye ajiuzulu kwa kushindwa kuwasimamia wenzake.
Mawaziri waliong’oka baada ya Rais Jakaya Kikwete
kutengua uteuzi wao kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo
na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete inatafsiriwa na wengi
kama njia ya kuwapoza wabunge na kumwokoa Pinda ambaye ikiwa atang’oka
itamaanisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili jana
zinasema wabunge 26 wametia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge litumie
mamlaka yake ya kikatiba kumng’oa Pinda kwa kumpigia kura ya kutokuwa na
imani naye.
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio
la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, endapo itatolewa hoja
kupendekeza hivyo.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kumpigia kura ya
kutokuwa na imani na waziri mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge
wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses
Machali alisema hili jana kuwa ukusanyaji saini za wabunge aliouanzisha
Ijumaa jioni unakwenda vizuri.
“Kung’oka kwa mawaziri wale wanne inatosha
kuthibitisha kuwa Pinda amepoteza uhalali wa kuwa Waziri Mkuu kutokana
na kushindwa kuwasimamia walio chini yake,” alisema Machali.
“Rais tunaweza kumuacha, lakini Pinda ndiye
mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali. Kama wapo mawaziri wameboronga ni
wazi na yeye anaingia moja kwa moja katika hilo kapu,” alisema na
kuongeza:
“Kama kweli tunataka taifa lisonge mbele kutoka
hapa tulipo ni lazima tumuondoe Pinda…….. amekuwa mpole mno, mzito
kufanya uamuzi na analea matatizo.”
Hata hivyo, alisema wabunge waliosaini fomu hiyo,
wote wanatoka kambi ya upinzani na kusema wabunge wengi wa CCM
aliowafuata kuwaomba watie saini wanaogopa au wanasita kufanya hivyo.
“Nataka niwaambie wabunge wa CCM hebu tusimame katika masilahi
ya umma… Serikali inapofanya vibaya wanaoumia ni wananchi wetu bila
kujali ni mwanachama wa chama gani,” alisema.
Pinda tayari amesema wazi kwamba yuko tayari
kujiuzulu wadhifa wake iwapo Rais Kikwete ataamua kumuondoa na kwamba
hata Rais asipochukua hatua hiyo ni ruksa kwa wabunge kutumia mamlaka
yao ya kikatiba ya kumuondoa kwa njia ya kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge wengine
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ambaye
alikuwa mwiba kwa Pinda bungeni alisema: “Haya ni mambo ya ajabu sana,
tutaendelea kubadilisha glasi lakini mvinyo ni uleule”.
Alisema uwajibikaji wa Serikali unaanzia kwa Waziri Mkuu na kusema anamuomba Rais atafakari ombi lake la kumfuta kazi Pinda.
“Tufike mahali tuambiane ukweli bila kumung’unya
maneno kama kweli tunataka kuisaidia nchi yetu na Serikali yetu ya Chama
cha Mapinduzi ambayo inapendwa na kuaminiwa na Watanzania,” alisema
Lugola.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa alisema anavyomuona Pinda na kutafsiri utendaji wake, anadhani
kuwa viatu vya uwaziri mkuu vinampwaya.
“Haiwezekani mara mbili ndani ya Bunge mawaziri
wang’oke halafu wewe ubaki… wanapoboronga katika utendaji wao lazima pia
umguse kiranja wao (Pinda) na hili bado tutalia nalo,” alisema Msigwa
na kuongeza:
“Tulitarajia Waziri Mkuu awe wa kwanza kutafakari
na kujipima kama kweli anastahili kubaki hasa baada ya madudu yale
ambayo yameichafua Serikali mbele ya umma.”
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
alisema wakati umefika kwa Waziri Mkuu, Pinda kukaa pembeni na kumwachia
Rais Kikwete aunde safu nyingine.
“Pinda ni mtu wangu. Tunaheshimiana na sina chuki
naye. Kwanza yeye ni mmoja wa watu ninaotuhumiwa kuwapa jimbo apite bila
kupingwa na kuniletea matatizo kwenye chama changu.
“Hivyo sina chuki naye maana pia anatoka kanda
yetu. Hata hivyo, hali ya sasa ya nchi inahitaji kupumua. Ampe nafasi
Rais aunde Serikali upya.”
Alisema kuna tatizo kubwa la uongozi ndani ya nchi na kuwa mambo
hayaendi licha ya juhudi mbalimbali pamoja na Bajeti ya Serikali
kuongezeka kila kukicha.
“Huduma hazifiki kwa wananchi. Serikali ni kama
haipo, nchi imevimba na inahitaji kupumua. Mwaka 1990 Rais Mwinyi (Ali
Hassan Mwinyi,) alikumbwa na hali kama hii na Warioba alijiuzulu ili
kumpa nafasi kuunda upya Serikali. Alimrudisha Warioba lakini mawaziri
wengi waliondoka,” alisema Zitto.
Aprili mwaka jana katika mazingira yanayofanana na
ya mkutano wa 14 wa Bunge uliomalizika Jumamosi, wabunge 74 wakiwamo wa
CCM walitia saini fomu ya kutaka kumng’oa Pinda.
Hata hivyo, aliepuka zahama hiyo, baada ya Rais
Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri mwezi mmoja
baadaye na kuwaondoa mawaziri sita na manaibu waziri wawili waliokuwa
wakishinikizwa kuachia ngazi.
Mawaziri hao walikuwa William Ngeleja (Nishati na
Madini), Mustafa Mkulo (Fedha), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii),
Omar Nungu (Mawasiliano), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Hadji
Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii). Manaibu walikuwa Dk Athuman Mfutakamba
(Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).
Kutoka Gazeti la Mwananchi.
Kutoka Gazeti la Mwananchi.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment