Dodoma.Kamati ya Bunge ya kuchunguza athari za
Operesheni Tokomeza Ujangili inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake leo,
ambayo inaelezwa kuwa imependekeza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya vigogo
kadhaa wa Serikali.
Taarifa ya kamati hiyo ndogo itasomwa leo wakati
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili itakapokuwa
inawasilisha taarifa yake ya utendaji kazi bungeni.
Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wajumbe wengi wa kamati hiyo ndogo wanatokana na
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili. Mmoja wa wajumbe wa
kamati hiyo ya uchunguzi alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa uchunguzi
wa kamati hiyo umegundua udhaifu mkubwa katika wizara na idara za
Serikali.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama
(CCM), James Lembeli imependekeza kuchukuliwa hatua kwa baadhi ya
maofisa waandamizi wa Wizara za Maliasili na Utalii na Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi. Mjumbe huyo alisema kwa upande wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, watakaoguswa na ripoti hiyo ni baadhi ya maofisa waandamizi
wanaosimamia wanyamapori na hata wale wa maliasili.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Novemba 25, mwaka huu
inawasilisha ripoti yake baada ya kumaliza kazi ya kuwahoji watu
mbalimbali wakiwamo mawaziri watatu ambao wizara zao zilihusika moja kwa
moja na operesheni hiyo.
Mawaziri waliohojiwa katika Hoteli ya Bahari
Beach, Dar es Salaam ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi
na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Shamsi Vuai
Nahodha.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana zilisema
kuna uwezekano mkubwa taarifa hiyo ‘ikamkaanga’ Dk Mathayo kutokana na
mapendekezo ya wabunge katika mkutano wa 13.
Wabunge walikerwa zaidi na kauli ya Dk Mathayo
alipopata fursa ya kuchangia taarifa ya Serikali kuhusu Operesheni
Tokomeza Ujangili na kuishia kuwapa pole wafugaji ambao mifugo yao
iliuawa kwa risasi.
Katika operesheni hiyo, wabunge walipaza sauti
wakidai wapo raia wasio na hatia waliouawa na kuteswa, huku mifugo
ikiporwa na mingine kama ng’ombe ikiuawa kwa kupigwa risasi.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola ndiye
aliyekuwa mwiba kwa mawaziri hao aliposema ana kitabu kilichosheheni
ushahidi dhidi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. Habari zaidi
zinasema kamati hiyo ya uchunguzi imelazimika kutofanyia shughuli zake
katika kumbi za Bunge ili kukwepa vishawishi kutoka kwa watu wa karibu
na vigogo wanaotuhumiwa.
“Wamejificha katika hoteli moja tangu waliporudi
Dodoma wiki iliyopita ili kuandaa ripoti yao kwa sababu hawataki
kuingiliwa ingiliwa na hili ndilo linalowatia hofu mawaziri,” alisema
mjumbe huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, pamoja na kasoro za
operesheni hiyo, ilisaidia kuwabaini maofisa walioko katika mtandao wa
ujangili na baadhi yao walikamatwa na nyara za Serikali.
Chanzo cha habari: Gazeti la Mwananchi
Chanzo cha habari: Gazeti la Mwananchi
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment