Matangazo:

kutangaza biashara yako hapa piga simu 0718865251 au email: excitetanzania.gmail.com

HABARI KAMILI

Tuesday, December 24, 2013

DK Slaa amtaka JK kuwawajibisha wakuu vyombo vya dola nchini

Igunga. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbroad Slaa, amehitimisha ziara yake wilayani Igunga na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza Ujangili (OTU).
Vile vile, amemuonya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kwa kusema kuwa anakabiliwa na tishio la kufukuzwa uanachana kutokana na kuwepo na vikaratasi vinavyogawanywa kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Barafu, Igunga, Dk Slaa alisema kwamba Rais Kikwete anapaswa kuwawajibisha iwapo hawatafanya hivyo ili kujijengea heshima katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wake uliobakia.
Alisema katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyowasilishwa Bungeni, Serikali na vyombo vya dola vimeumbuka kutokana na kubainika kuwa vilihusika katika kuwatesa raia, kuwaua ikiwa ni pamoja na kupora mali zao, hivyo kwa vile watekelezaji walikuwa ni idara ya usalama wa Taifa, Polisi na Jeshi la Wananchi bado wakuu wake wanapaswa kujiuzulu kutokana na aibu hiyo.
“Kule Serengeti mkoani Mara walimkamata kijana wetu, tena Diwani wa Chadema na kumlazimisha kukiri kuwa alikuwa akimiliki bunduki na kuwinda tembo, alipokataa walimpiga shoti ya umeme, wakamwekea waya wa baiskeli na kuusokota, lakini kule Babati wamemkamata mama wakidai kuwa alikuwa akiua tembo na kumbaka kwa zamu,” alieleza Dk Slaa.
Alisema kwamba mateso haya yanafanyika sasa na vyombo vya dola baada ya kufanywa kwa muda mrefu na watendaji wa vijiji, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, lakini licha ya kwamba njia ya kuondoa kero hizo za manyanyaso kwa wananchi hazihitaji fedha, lakini bado Serikali imekuwa ikishindwa kuchukua hatua.
Alisema watu wanabambikiwa kesi za mauaji kwa makusudi, Serikali ipo ikiangalia pamoja na vyombo vya usalama wa Taifa, hivyo kuwataka wakuu wake nao kufuata njia za mawaziri wanne kwa kujiuzulu ili kulinda hadhi ya taasisi zao.
“Polisi walikamata vijana wetu wa Chadema wakati walipokuwa wakitaka kutubambikia kesi ya ugaidi, waliwapeleka kule Tabora waliwatesa na umeme mateso makali sana, waliwachanachana kwa visu vya bunduki sehemu zao za siri na kuwawekea waya, mateso haya ni makali na yamefanywa kwa vijana ambao wameoa juzi, bora hata wangefanya kwangu mimi mwenye umri mkubwa,” alieleza kwa masikitiko.
Alipokuwa katika Wilaya ya Nzega, Dk Slaa, alimuonya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe  kuwa anakabiliwa na tishio la kufukuzwa uanachama kwa kile kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Nzega Mjini alisema chama kimepokea taarifa za mpango wa kundi la watu ambao wanasadikiwa kuwa wafuasi wa Zitto kupitisha karatasi na kusainisha majina ya wanachama kwa lengo la kuandaa pingamizi dhidi ya uamuzi wa chama jambo ambalo alisema litamponza.
Share it Please

Excite Media

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.

0 comments:

Post a Comment

Copyright @ 2013 SHAUKU BLOG. Designed by Templateism | Love for The Globe Press