Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za umeme ambazo zimepanda
kwa kuzingatia makundi tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei mpya
zitaanza kutumika Januari Mosi, 2014 mpaka Desemba 2016. Hata hivyo,
alisema mabadiliko ya bei yanaweza kutokea katikati ya kipindi hicho cha
miaka mitatu.
Pia alisema bei hizo za umeme zitakuwa
zikirekebishwa kila baada ya miezi mitatu kutokana na mabadiliko ya
kiwango cha bei za mafuta, mfumuko wa bei, mabadiliko ya thamani ya
fedha sanjari na upatikanaji wa ruzuku kutoka serikalini.
Alisema kutokana na matarajio ya kuanza kuzalisha
umeme wa gesi, Ewura imeiagiza Tanesco kufanya utafiti wa kutathmini
mahitaji ya wateja wake katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Bei mpya ya umeme
Ngamlagosi alisema mwananchi wa kipato cha chini
anayetumia uniti (0-75) kwa mwezi, atalazimika kulipia Sh100 kwa uniti
ukilinganisha na Sh60 iliyokuwapo awali.
Ongezeko lipo pia katika kundi linaoitwa T1 la
watumiaji wakubwa wa umeme wa nyumbani, ambao watalipia Sh306 kwa uniti
ikiwa ni ongezeko la Sh85 ya bei iliyopo sasa.
Alisema katika kundi la T2 la wateja wakubwa
wanaopimwa kwenye matumizi ya uniti 7,500, malipo ya uniti moja
yamefikia Sh205 ikiwa ni ongezeko la Sh73 kutoka bei ya sasa.
“Kundi jingine la T3-MV ambao ni wateja wa viwanda
vikubwa, litaanza kulipia Sh166 kwa uniti ikiwa ni ongezeko la Sh45 ya
bei ya sasa pamoja na kundi la T3HV lililounganishwa kuanzia voti 66,000
na zaidi ambalo litaanza kulipia Sh159 kwa uniti ikiwa ni ongezeko la
Sh53,” alisema Ngamlagosi.
Masharti kwa Tanesco
Akizungumzia masharti yatakayoendana na
utekelezaji wa bei hiyo mpya, Ngamlagosi alisema Bodi ya Wakurugenzi ya
Ewura imeliagiza shirika hilo kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia mitambo
yenye gharama nafuu huku ikilazimika kuwasilisha ripoti ya utekelezaji
wake kila mwezi.
“Pia italazimika kuwasilisha ripoti kila baada ya
miezi mitatu kuhusu viashiria vya takwimu za ubora na uhakika wa umeme,
pia itakuwa ikiwasilisha ripoti kila baada ya miezi mitatu kuhusu
ukusanyaji wa madeni yake ili kuongeza mapato ya shirika,” alisema
Ngamlagosi.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Tanesco kuwasilisha
maombi Ewura ya kurekebisha bei za umeme, ikipendekeza kupandisha bei
hizo kwa asilimia 67.87 kwa lengo la kuiwezesha kujiendesha kutokana na
changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma.
Ngamlagosi alisema mamlaka hiyo imepata ufumbuzi
wa kunusuru shirika hilo katika maeneo mawili ikiwamo kuongeza bei ya
gharama za umeme na shirika kupatiwa mkopo wa gharama nafuu.
Alisema uamuzi huo unatokana na uchambuzi
uliofanywa na Ewura katika maeneo ya kifedha na kiufundi ndani ya
Tanesco ili kujiridhisha na maombi hayo, pia kuangalia uwezo wa
kutekeleza majukumu yake.
“Baada ya hapo, Ewura ilibaini kuwa hali ya
kifedha Tanesco si nzuri kwani hasara imeendelea kuongezeka kutoka
Sh47.3 bilioni kwa mwaka 2010 mpaka kufikia hasara ya Sh223.4 bilioni
kwa mwaka 2012,” alisema Ngamlagosi.
Pamoja na upungufu wa kiufanisi, mamlaka hiyo
imesema kuwa ilibaini sababu ya kuongezeka hasara kuwa ni ongezeko la
gharama za uzalishaji wa umeme ambao Tanesco inanunua kutoka kwa
wazalishaji binafsi na hivyo kushindwa kulipa madeni yanayofikia kiasi
cha Sh456.8 bilioni.
Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi
Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment