Ulimwengu mzima unatambua kwamba hakuna nchi iliyowahi kuendelea
bila wananchi wake kuwa na elimu. Maendeleo yote yametokana na elimu
sahihi iliyojaa maarifa, ubunifu, uwezo mkubwa wa kufikiri na kuvumbua
dhana mpya.
Elimu hii ni ile inayojenga ujuzi na ufundi wa
aina mbalimbali, inayojenga kujiamini, kudadisi na kutumia fursa
zilizopo kutafuta ufumbuzi wa matatizo.
Ukweli huu ndio unaoisukuma jamii kubwa kuwekeza
katika elimu. Tena siyo bora elimu tu, bali ni elimu sahihi inayolingana
na mahitaji ya jamii. Kuna ukweli usiopingika kwamba wafadhili wametoa
pesa nyingi kusaidia nchi maskini ikiwemo Tanzania, lakini bado umaskini
umetamalaki.
Pamoja na misaada hii, Tanzania imebarikiwa
utajiri mkubwa mno ambao kama ungetumika kwa haki na usawa, ungepunguza
umaskini kwa kiwango kikubwa.
Jamii kubwa ya Watanzania inaishi ndani ya lindi
la matatizo lukuki ambayo nchi nyingi walishayatatua miongo kadhaa
iliyopita. Wenzetu sasa wanatafuta maarifa mapya ya kuibadili dunia hii
wapendavyo, kwa kurahisisha kila kitu kwa teknolojia na uvumbuzi mpya.
Hii yote ni nguvu ya elimu!
Kwa mantiki hiyo, suala la kuwekeza katika elimu
sahihi haliepukiki na linapaswa kutiliwa mkazo na kila mmoja wetu kwa
kuzingatia umuhimu wake.
Hata hivyo, kwa sasa tunahitaji kuwekeza kisasa na
kibunifu katika elimu, sio kuwekeza kimazoea tu kunakoacha nyuma
maarifa ya wanafunzi na kukimbilia vyeti, idadi na mitihani. Uwekezaji
wa kweli katika elimu ni kufanya kile mwanafunzi anapaswa kupata awapo
shule ili aweze kupambana na changamoto zinazoikabili jamii
inayomzunguka. Siyo kufanya kile wanasiasa wanachotaka kuona.
Elimu ni mchakato wa kuwapatia wanafunzi maarifa
stahiki, sio kuwafurahisha wanasiasa. Kumfurahisha mwanasiasa na kuacha
mwanafunzi akiwa hana maarifa wala ubunifu wowote ni usaliti kwa maelfu
ya watoto wa Tanzania.
Hali hii inaibua changamoto nyingi katika sekta ya
elimu kama vile: kuwa na mitalaa isiyoelekeza wala kukazia kumjenga
mwanafunzi kupata maarifa, ujuzi na stadi za aina mbalimbali
zitakazowasaidia wanafunzi kuishi pindi wamalizapo shule.
Mitalaa ya sasa imebuniwa ili kuufanya usomi
uonekane ni kufaulu mtihani na kukumbuka dhana rahisi tu. Mitalaa
haiwafundishi au kuwapa vijana uwezo wa kutatua matatizo ili kujenga
nguvu ya kupambana na changamoto zinazoikabili jamii. Wanakaririsha
nadharia tu ambazo haziwajengei maarifa wala ujuzi wowote.
Mitaala imetungwa na wataalamu wachache bila
kuzingatia mahitaji ya jamii. Unakuta mada nyingine katika masomo
hazihitajiki kabisa. Wanafunzi wanajikuta wamejazwa majuzuu ya nadharia
zisizohitajika wala kutumika. Matatizo ya jamii yanabaki palepale.
Walimu nao hawatoshelezi mahitaji, kuwa na walimu
wasio na sifa za ualimu na waliokata tamaa ni hali ya kawaida kwa
Tanzania kwa sasa. Kuna upungufu mkubwa wa walimu Tanzania. Wengi
wanaacha kazi na wachache waliopo wamekata tamaa kutokana na sekta ya
elimu kukosa mvuto na kukithiri kwa siasa kwenye elimu.
Kutokana na hili walimu wengi hawana moyo wa kufundisha.
Hawatumii kabisa vionjo vya saikolojia ya ualimu. Na matokeo yake
wanafunzi wanakosa maarifa na malezi ya walimu. Wengi wanafeli mitihani
na hatimaye kufeli maisha.
Motisha kwa walimu, kuwajali, kuwasimamai na
kuwawajibisha walimu na kuwathamini ni jambo la muhimu kuelekea elimu
bora. Bila kuwafanyia haya walimu hakuna elimu bora. Kuwahadaa walimu
kila siku kwa ahadi zisizotekelezeka ni kudhoofisha maendeleo ya Taifa
na kuliweka rehani kwa watu mbumbumbu!
Walimu wamekuwa wakifundisha kupitia unaoitwa
mfumo wa “ubao –chaki” unaowafanya wanafunzi kuwa ni vikapu tu vya
kupokea maelezo ya mwalimu bila kuchagiza kufikiri na kuvumbua kitu
kipya.
Katika karne hii ya maarifa na changamoto nyingi
mfumo huu haufai. Mbinu shirikishi zinazowapa muda na fursa wanafunzi
kujadili wenyewe na kutoa mawazo yao kwa uwazi ndio sahihi.
Mbinu hizi zinaamsha ari ya kujifunza, zinaamsha
udadisi, ubunifu, fikra yakinifu na kukuza uhodari wa kutafuta maarifa
hata kama hawapo shule.
Siku hizi ni kawaida kuona uamuzi wa mtu mmoja
unatawala shughuli nzima za taasisi fulani. Na baadhi ya viongozi
wamegeuka madikteta. Hali hii imeondoa uharaka wa kuleta mabadiliko
katika taasisi zetu za elimu. Kwa mfano, hakuna mikakati ya kifikra na
ki mipango ya kuifanya shule kuwa mahali salama pa kujifunza na kuibua
vipaji vya watoto. Pengo hili bado halijafanyiwa juhudi za dhati
kuzibwa.
Kwa sasa, mtoto wa masikini anayelilia elimu
imkomboe, anahitaji mfumo mzuri utakaotoa dira na dhamira ya kweli
kuifanya elimu kuwa ni haki ya msingi kwa kila mtoto, sio watoto wa
viongozi na mabepari tu.
Tunahitaji kubuni mfumo bora wa elimu utakaokuwa
na uongozi imara unaojua mabadiliko na kufanyakazi kibunifu na
kushirikiana. Mfumo wa namna hii utawajengea wanafunzi uhuru wa kutafuta
maarifa, kutoa maoni, kusikilizwa pamoja na kupendekeza mikakati
mbalimbali ya kuboresha taalumu yao.
Tunahitaji dira ya elimu inayotufaa, inayoelekeza
kwenye malengo ya elimu. Na mchakato mzima wa kujifunza utapitia katika
dira hiyo. Dira inayoishi na kufanyakazi, siyo dira ya kwenye nembo za
sare za wanafunzi, kwenye nyaraka za Serikali na kwenye vitabu tu,
lakini hazifanyi kazi. Dira iliyokufa nayo inaua elimu!
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment