Wengi wanaitazama hatua iliyochukuliwa na viongozi wa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuridhia kuanzishwa
kwa sarafu ya pamoja ni sawa na kusukuma tofali kwenye kina kirefu cha
maji bila kuwa na matarajio ya kulifikia tena tofali hilo.
Kwa mujibu wa malengo ya jumuiya hiyo, kufikia
mwaka 2023 mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki yatakuwa
yamefikia shabaha ya kuwa na sarafu moja hatua ambayo itafungua uwanja
mpya wa ushirikiano wenye nguzo tatu.
Kukamilika kwa shabaha hiyo kutategemea pia utashi wa kisiasa kutoka kwa nchi wanachama bila kujali idadi ya raia wake.
Iwapo shabaha hiyo itafanikiwa kama ilivyopangwa
basi Kanda ya Afrika Mashariki itakuwa imeingia kwenye rekodi mpya kwa
kuwa itakuwa Jumuiya ya pili kuwa na sarafu moja ya fedha ikitanguliwa
na ile ya Umoja wa Ulaya.
Juhudi kama hizo za kuwa na safaru za pamoja
zimewahi kufanywa na nchi zilizoko kwenye ushirikiano wa kibiashara kwa
nchi za Asia ya mbali, lakini hazikuzaa matunda.
Mkataba wa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama
‘Maastricht Treaty’ ulisainiwa kwa mara ya kwanza Februari 7, mwaka 1992
na baada ya kupita mwaka mmoja utekelezaji wake ulianza kazi. Umoja huu
ulitimiza miaka mingine saba kutimiza ndoto ya sarafu moja ‘euro’.
Kwa kuzingatia biashara ya kubadilishana fedha na
mtiririko wa biashara katika masoko ya kimataifa, sarafu ya euro
inatajwa kuwa ni miongoni mwa sarafu zilipata mafanikio makubwa kwa
kipindi kifupi baada ya kuanzishwa. Inasadikika baadaye huenda sarafu
hiyo ikawa na nguvu katika soko la kimataifa.
Maktaba
Mkataba wa kuanzishwa kwa sarafu moja kwa nchi za
Afrika Mashariki umesiniwa ikiwa imepita miaka 21 tangu kuasisiwa kwa
mkataba wa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya. Pamoja na hatua hiyo
iliyoanzishwa na viongozi wa Afrika Mashariki inatazamwa ikiwa ni sawa
na kutosa tofali kwenye kina kirefu, lakini wanauchumi wanaona kwamba ni
wazo linalokaribiana na ukweli.
Mbali na hayo kugundulika kwa rasilimali ghafi
katika baadhi ya mataifa, ni moja ya vigezo vinavyofanikisha ndoto ya
kuwa na sarafu moja. Kimsingi sarafu ya pamoja inaziwajibisha nchi
wanchama kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kudhibiti kuporomoka
kwa uchumi.
Eneo la Afrika Mashariki ambalo linakadiriwa kuwa
na idadi ya watu wanaofikia milioni 135 lina uwezo wa kuzalisha bidhaa
zitakazohimili ushindani wa kimataifa. Tanzania pekee ambayo kwa sasa
ipo kwenye hatua za mwisho za kuchimba gesi na mafuta ina uwezo wa
kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja na kuzika kasumba ya miaka mingi ya
utegemezi wa misaada kutoka mataifa yenye nguvu ya kigeni.
Iwapo mradi unaozinduliwa na Kenya wa ujenzi wa
reli kwa msaada wa Serikali ya China utakamilika kwa wakati, mafuta
yaliyogunduliwa hivi karibuni nchini Uganda na Kenya-utavutia wawekezaji
wengi wa kigeni na kutoa msukumo mpya wa kibiashara miongoni mwa nchi
wanachama. Reli hiyo itapitia katika baadhi ya nchi wanachama.
Chanzo cha habari: Mwananchi
Chanzo cha habari: Mwananchi
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment