Zanzibar.Baba wa Taifa alipendelea sana kuitwa
Mwalimu, kazi aliyoanza kufanya kabla ya kuwa Rais wa kwanza na hadi
anastaafu urais jina la Mwalimu hakuliacha hadi mauti yalipomkuta.
Hii inakuwa ni vigumu kwa mtu aliyetumikia nafasi
nyingi kwa nyakati tofauti na kwa mafanikio mazuri, nasema mazuri kwa
sababu Jaji Augustino Ramadhani aliyestafu Ujaji Mkuu alipaswa pia
kuitwa Brigedia Jenerali kwa kuwa pia alilitumikia Jeshi hadi kufikia
ngazi hiyo ya Brigedia Jenerali kabla ya kuitwa katika sekta ya sheria
na kutumikia Mahakama hadi kufikia ngazi ya juu kabisa ambayo pia wengi
hupenda kuandikwa kwa vyeo walivyowahi kutumikia na kwa sasa amepewa
kazi ya ukasisi.
Mbali na kustaafu ujaji, wiki iliyopita alipewa
kazi ya ukasisi, alitawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa
la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar na hivyo kustahili kuitwa cheo
cha Mchungaji Augustino Ramadhani.
Mchungaji Augustino aliiambia Mwananchi kuwa
alizaliwa Visiwani Zanzibar, Mtaa wa Kisima Majongoo kwenye familia ya
watoto wanne wa Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Anna
Constance Masoud akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo, aliishi kwa
miaka mitatu Visiwani huko na kisha alikuja Tanzania Bara (Tanganyika)
akiwa na umri wa kuanza masomo hadi alipohitimu masomo ya sekondari
katika Shule ya Wavulana Tabora na wakati akiwa sekondari ndipo
alilpojifunza kupiga kinanda akirithi kipaji cha babu yake Augustino
Ramadhani.
Jaji Ramadhani alihitimu elimu ya sekondari mwaka
1965 na kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
katika fani ya sheria hadi mwaka 1970 alipojiunga katika Jeshi la
kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, baadaye aliajiriwa katika Jeshi la
Ulinzi la Wananchi (JWTZ) alikofanya kazi za sheria.
Mafanikio zaidi
Alifafanua kuwa aliitwa na aliyekuwa Rais wa pili
wa visiwa hivyo, Alhaji Aboud Jumbe mwaka 1978 na kumteua kuwa Naibu
Jaji Mkuu kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwaka huo huo aliitwa
tena jeshini kwa ajili ya kushiriki vita ya Kagera, alipelekwa Uganda na
kukaa kwa zaidi ya miezi kumi.
Baada ya vita kumalizika alirudi Tanzania
kuendelea na kazi katika sekta ya Sheria na mwaka 1980 aliapishwa kuwa
Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Anasema, mfumo wa Mahakama Visiwani haukuwa wa
kisheria na alifanikiwa kuubadilisha na kuweka mfumo wenye ngazi za
Kimahakama kutoka Wilaya, Mkoa hadi Mahakama Kuu. Anabainisha kuwa hii
ilitokana na kutokuwepo na watu waliosomea sheria ili kuajiriwa katika
sekta ya sheria.
“Nilifanikiwa kuondoa mfumo wa mabaraza (Peoples
Court) na kuweka mfumo wa mahakama uliofuata ngazi za kimahakama na
mahakama ya Rufaa haikuwepo kabisa”, anasema.
Pia aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa
mwaka 1989, mwaka 1990 alihamia jijini Dar es Salaam na Mwaka 1993 hadi
2003 aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania
Bara na mnamo mwaka 2002-2007 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar na katika kipindi hicho hicho alikuwa mmoja wa Majaji
sita wa Mahakama ya Afrika Mashariki, pia alikuwa ni mmojawapo wa Majaji
11 waliochaguliwa na Marais wa Afrika kwa ajili ya kuitumikia Mahakama
ya Afrika ya Haki za Binadamu na ndipo mwaka 2006 alipoteuliwa na Rais
Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Baada ya kustaafu kazi ya Ujaji Mkuu mwaka 2010,
Jaji Augustino Ramadhani alikataa kuendelea na kipindi kingine baada ya
kufanikiwa kufafanua kifungu kinachokataza Jaji kuendelea na kazi ya
Ujaji baada ya umri wake wa kustaafu na kuendelea kwa mkataba wa
ajira, ila anaruhusiwa kuongeza kipindi kimoja tu hata kama bado anazo
nguvu za kutumikia Taifa.
Mara baada ya kusimikwa kuwa Mchungaji anasema, hakuna tofauti
kati ya kazi ya Mahakama na kazi ya Uchungaji kwani zote ni kazi za
kufanya maamuzi ya watu wanaodai wapatiwe haki na kubainisha kazi za
mahakama ukiamua umeamua ila za kanisa zinataka makubaliano na
maridhiano japo zote ni kazi za Mungu.
“Kazi hii ya uchungaji mimi sikuifikiria hata siku
moja kwamba nitaifanya ingawa nilisomea nchini Uingereza na kutunukiwa
stashahada. Pia nilikuwa nikishiriki katika shughuli za madhabahuni
hasa wakati wa kuwasimika maaskofu kwa kuwa nilikuwa mwanasheria wa
kanisa hili hadi nilipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu ndipo nilipoamua kuacha
wadhifa huo ili kuepuka migongano,”anasema Jaji Ramadhani.
Atafutwa
“Askofu alinifuata mara kwa mara ingawa nilikuwa
nikimkatalia lakini mwisho nilikubali kwa kuona kuwa ni sauti ya Mungu
iliyokuwa ikiniita kupitia kwake na ndio leo hii baada ya kutumikia
ushemazi kwa zaidi ya miezi sita nimesimikwa rasmi kuwa mhudumu wa
madhabahuni.”
Kwa upande mwingine Jaji anasema, lengo lake
lilikuwa baada ya kustaafu akafundishe na lengo hilo limetimia kwani pia
kwa sasa ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Tumaini Iringa anapofundisha
sheria.
Pia itakumbukwa kuwa wiki hii amekamilisha kazi ya
kuunda rasimu mpya ya katiba alipoteuliwa mwaka jana kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Hali ya Zanzibar
Akizungumzia hali ya vugu vugu la hali ya visiwani
humu kuhusu kushambuliwa kwa viongozi wa dini na kuharibiwa kwa nyumba
za ibada anasema tangu miaka ya nyuma akiwa mdogo anakumbuka jinsi
walivyokuwa wakishirikiana vizuri na majirani zao kuadhimimisha sikukuu
za kidini bila kujali tofauti ya za dini.
“ Nakumbuka wazazi wangu walikuwa wanamwita
Mwislamu kuja kuchinja kuku ili wasikwazike wanapokaribishwa kujumuika
katika chakula, kwa kuwa walijua kuwa nyama wanayokula imechinjwa kwa
taratibu za dini yao na haitamkwaza na wao pia walikuwa wakitualika
kwenye sikuku zao na tulikuwa tukifurahia pamoja.”
Mwananchi pia ilishuhudia amani iliyokuwepo wakati
misa ya kumwapisha Jaji Mstaafu Augustino Ramadhani ilipokuwa
ikifanyika na hakuwa na uvunjivu wa aina yoyote ya amani licha kuwepo na
ulinzi wa kawaida na hakukuwa na Polisi kama ilivyokuwa wakati wa
mkesha wa Siku Kuu ya Krismasi.
Wageni walikuwa wengi na kanisa lilijaa watu waliokuja kushuhudia tukio hilo la kusimikwa kwake.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment