Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti ya Kamati ya
Maliasili, Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi bungeni mjini
Dodoma, imewang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao
zilishindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni
jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya
Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano
akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Dk Mathayo David Mathayo.
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni
Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa 2:09
usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo
iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni
Mbunge wa Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi ni
mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais
Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii,
yaliyotokea yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii
kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida
kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika
aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo
hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa ripoti
hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na
kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo
akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia
mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo ya wafugaji aliyopewa na Rais
Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa
mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi
(Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali
ushauri wa Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi
wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati yake,
Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na
Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea
kwenye mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya
wizara hiyo ni kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali
izichunguze simu zao kuanzia leo.”
Michango ya wabunge
Awali hali ya hewa ndani ya kumbi wa Bunge jana ilichafuka baada
ya wabunge kuchangia kwa hisia kali, wakitaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda
kujiuzulu sambamba na mawaziri wengine watatu.
Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ni wa Maliasili na
Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha.
Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), alienda
mbali zaidi na kutaka Bunge livunjwe endapo Waziri Mkuu na mawaziri hao
watatu watakataa kujiuzulu kwa lengo la kung’ang’ania madaraka.
Michango ya wabunge hao ilitokana na ripoti ya
kamati ndogo ya uchunguzi ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
chini ya Mwenyekiti wake, James Lembele iliyowasilishwa bungeni jana.
Ripoti hiyo inayohusu Operesheni Tokomeza Ujangili
(OTU), ilibainisha kuwapo mauaji ya watu 13 na askari sita, utesaji wa
kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.
Hata hivyo pamoja na kamati ya Lembeli kumtaka
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David apime kama bado
anastahili kuongoza wizara hiyo, wabunge walimsafisha.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema),
alisema hakuna jinsi ya kuonyesha namna wabunge walivyokasirishwa na
vitendo hivyo zaidi ya Serikali nzima kwa maana ya Pinda kujiuzulu.
“Naomba Waziri Mkuu uchukue ‘political
responsibility’ (uwajibikaji wa kisiasa) na siyo kwamba kwa kufanya
hivyo anahusika la hasha… Kama hachukui hatua Bunge libebe dhamana
hiyo,” alisema.
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisema ripoti
hiyo ya Lembeli imetaja kuwapo baadhi ya wabunge wanaotuhumiwa kwa
ujangili na kuhujumu OUT akitaka kamati iwataje ndani ya Bunge.
“Bungeni kazi yetu, sisi Wabunge ni kuisimamia
Serikali kwa hiyo wale wabunge waliotajwa kwenye ripoti watajwe ili nao
wawajibike ili Bunge letu liwe na nia thabiti ya kuisimamia Serikali,”
alisema Mbatia.
Wabunge waliochafua zaidi hali ya hewa kutokana na
michango yao ya hisia kali dhidi ya Pinda ni Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola (CCM), na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa.
Lugola alisema makosa ya operesheni hiyo yalianza
mapema wakati operesheni ya kijeshi ilipopelekwa kwa raia na kusema;
“Hainiingii akilini kwamba aliyekuwa ana command (kutoa amri) ni
mwanajeshi.”
“Wakati operesheni hii ikitokea wanawake wanabakwa na watu
wawili…Watu wameteswa, mwanaume mwenzetu amelazimishwa kufanya mapenzi
na mti Waziri Mkuu ulikuwa wapi haya yakitokea?” alihoji.
Lugola aliongeza; ”Kwa utaratibu wa nchi yetu
tumekupa kila aina ya usafiri kuanzia helikopta, ving’ora kila wakati
vinalia ulikuwa wapi Waziri Mkuu wakati mambo haya machafu yanatokea?”
Alisema Vuai hawezi kupona katika suala hilo kwa
kuwa wanajeshi ndiyo waliobaka, kuua na kujeruhi na ndiyo walioua mifugo
kwa risasi na kwamba atapona katika Bunge hilo mbele ya haki hatapona.
Vivyo hivyo alisema Dk Nchimbi hawezi kupona katika kashfa hiyo kwa vile
askari polisi ndiyo walioua, kubaka, kuwapa watu vile na kuua mifugo
akisema; ”Utaponea wapi Dk Nchimbi?”
Lugola alisema pamoja na ripoti ya kamati kumnukuu
Kagasheki akidai alinyang’anywa mamlaka yote katika utekelezaji wa OTU,
akihoji ni waziri wa namna gani aendelee kukalia kiti cha uwaziri.
“Nimeisoma ripoti hii hakuna mahali Dk Mathayo
alipohusika anataka kutolewa kafara… Mifugo yake imeuliwa hahusiki na
sera yeye anahusika na wafugaji waliouawa pamoja na mifugo,” alisema
Lugola.
Hata hivyo Lugola alisema Dk Mathayo anahusika na
uzembe kwa kuwa wafugaji imeuawa, mifugo imeuawa na kuhoji waziri huyo
alikuwa wapi wakati hayo yakitokea ndani ya Tanzania.
“Naendelea kumshauri Rais kama tunaitakia mema
nchi hii na kama tunataka CCM kiendelee kuaminiwa na Watanzania, Rais
amfukuze Waziri Mkuu mara moja,” alisisitiza mbunge huyo.
Aliongeza kusema; “vv Mawaziri wake hao
hawawezi kukwepa hili, watu wanachukua ‘political responsibility’ kwani
Maige (Ezekiel) alichukua Twiga porini?” alihoji na kuongeza kusema;
“Kama tunataka tuwe na Bunge lenye viwango, Bunge
lisilokuwa na ‘double standard’ (upendeleo) na nyinyi watu wameua watu
na nyinyi lazima muondoke ndiyo tutajenga heshima ya nchi hii,” alisema.
Lugola alenda mbali na kusema endapo Rais
atashindwa kumfukuza Pinda katika wadhifa wake huo, yeye atakuwa wa
kwanza kupeleka hoja bungeni ili wabunge wapige kura ya kumng’oa Waziri
Mkuu.
Kwa upande wake, Msigwa alisema wabunge
wanapopendekeza Waziri Mkuu aachie ngazi hawana chuki naye, lakini kwa
madudu yaliyotokea chini ya usimamizi wake ni lazima awajibike.
“Na kama mnatuheshimu, mheshimiwa Waziri Mkuu
ungekuwa unatayarisha makaratasi saa hizi unaandika barua za kujiuzulu,
tukufanyie sherehe ya kukuaga na nyie wa chini yake mfuate,” alisema.
Msigwa alienda mbali zaidi na kumnyooshea kidole Vuai kwamba ana
rekodi mbaya kuanzia Zanzibar na kwamba dhambi ya damu ya mauaji ya
raia huko Pemba inamlilia na kumfuata hadi Bara.
“Hata sisi tunasema hamkuhusika ‘direct’ (moja kwa
moja) lakini hapa tunazungumzia uhai wa watu na watu waliokufa siyo
wanachama wa CCM wala wa vyama vya upinzani…Tutangulize utaifa,”
alisema.
Mbunge huyo alisema siku zote cheo ni dhamana na
kwamba wasingependa Chadema itakapochukua nchi iwapeleke mawaziri hao
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, iliyopo The Heague nchini Uholanzi, kwa
kuwa hawatapona.
Lekule ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho
aliposema endapo Bunge litamaliza mkutano wake huo bila kuwapo mawaziri
watakaowajibika, basi Rais alivunje Bunge ili ufanyike uchaguzi
mwingine.
Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.
Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment