Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba
itakabidhi rasimu ya pili ya Katiba kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka huu.
Makabidhiano hayo yatafanyika katika hafla
itakayofanyika katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam baada ya Tume
kumaliza kazi yake ya kuiandaa.
Rasimu hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi
saba tangu tume hiyo ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa
katika Mabaraza ya Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2
mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 20 (2) ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, mara baada ya Rais kukabidhiwa rasimu hiyo,
itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani
ya siku 31.
Pia katika kipindi hicho, Rais anatakiwa kuitisha
kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu
iliyopendekezwa. Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa kuwa Bunge
la Katiba litaanza vikao vyake Februari, 2013.
Taarifa ya Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid
iliyotolewa jana ilieleza kuwa Tume hiyo itakabidhi rasimu hiyo kwa
Marais Kikwete na Dk Shein katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na
wananchi wa kawaida.
Tume hiyo ilitakiwa kumaliza kazi ya kuandaa
rasimu ya pili Desemba 15 mwaka huu lakini Rais Kikwete aliiongezea siku
14 zaidi hadi Desemba 30, mwaka huu.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete kuiongezea muda tume
hiyo ilikuwa ya pili. Mara ya kwanza iliomba kuongezewa muda wa siku 45,
kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu. Kabla ya kuomba
kuongezewa muda mara ya kwanza, ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba
30.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza Tume
hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa inampa Rais mamlaka ya
kuiongezea muda usiozidi siku 60.
Hatua ya Rais kuiongezea muda kwa mara ya pili,
ilitafsiriwa kama kutoa fursa kwa wajumbe wake kujipanga upya baada ya
kifo cha mwenzao, Dk Sengondo Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu
huko Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga.
Mambo yanayosubiriwa kwa hamu
Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na tume hiyo katika rasimu ya
kwanza ambayo yanatarajiwa kuibua mjadala iwapo yatabaki kama yalivyo,
kuondolewa au kuongezwa katika rasimu ya pili ni pamoja na muundo wa
Muungano.
Baada ya Tume kupendekeza mfumo wa Muungano wenye Serikali Tatu, watu wa kada mbalimbali walitoa maoni tofauti.
Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba alitetea
kuwa katika mazingira ya sasa, mfumo wa Serikali Tatu haukwepeki kwa
maelezo kuwa utasaidia kuondoa hofu ya Zanzibar kumezwa kama
ilivyojengeka kwa Wazanzibari wengi na wananchi wengine wa Tanzania
Bara.
Mambo mengine yaliyomo katika rasimu ya kwanza
yaliyozua mjadala ni pamoja na mawaziri kutokuwa wabunge, kufutwa kwa
viti maalumu, wabunge kugombea ubunge kwa awamu tatu pekee.
Mengine ni kuhojiwa kwa matokeo ya urais
mahakamani, kufutwa kwa nafasi ya waziri mkuu, kupendekeza waziri yeyote
mwandamizi ateuliwe kukaimu nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ikiwa Rais na Makamu wake hawapo nchini kutokana na sababu
zozote zile.
Pia ilipendekezwa jumla ya wabunge wawe 75, kwa
maana 50 watoke Tanzania Bara, 20 Tanzania Visiwani na watano watoke
kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais.
Katika rasimu hiyo, pia imependekezwa kusiwepo na
uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi yake ni ya mgombea binafsi. Kama
ni ya chama cha siasa, basi nafasi hiyo ijazwe na mtu kutoka chama
chake.
Kuhusu madaraka ya Rais, tume hiyo ilipendekeza
yabaki kama yalivyo, kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia
ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, rasimu hiyo ya kwanza
ilipendekeza jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (Nec), libadilishwe na
kuwa Tume Huru ya Uchaguzi.
Pia ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu
(Supreme Court). Ilisema majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani
watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa
Mahakama.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment