Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetoa Rasimu ya Pili ya Katiba ikiwa na mambo sita mpya, huku
ikiendelea kupendekeza Muungano wa Serikali tatu na kurejea kwa nchi ya
Tanganyika.
Rasimu hiyo ya Pili ambayo imetolewa miezi saba
baada ya Rasimu ya Kwanza, ilikabidhiwa jana kwa Rais Jakaya Kikwete na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika hafla iliyofanyika
kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Akizungumza kabla ya
kukabidhi rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema ina Ibara 271, tofauti na
ile ya kwanza iliyokuwa na Ibara 240.
Alisema ripoti ya rasimu hiyo pia ina maoni ya
wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, sera, sheria na utekelezaji maoni
ya Mabaraza ya Katiba, takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi,
makala za utafiti kuhusu mabadiliko ya Katiba na viambatanisho vya
ripoti ya mabadiliko ya Katiba.
Mambo mapya
Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho baada ya mchakato
wa Mabaraza ya Katiba yaliyokutana kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2
mwaka huu ni kuongezwa kwa vipengele kuhusu haki za binadamu.
Miongoni mwao ni haki ya kutoa na kupata habari.
Pia imetaja haki za makundi maalumu yakiwamo ya watoto, vijana, wazee,
walemavu na wanawake.
Kuhusu uraia, Jaji Warioba alisema imependekezwa
uraia wa Tanzania kuwa mmoja tu na kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na
wa kujiandikisha wa nchi moja. Alisema imependekeza pia kutoa fursa kwa
uraia wa nchi mbili.
Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya
uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa
kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Aidha, alisema rasimu hiyo imependekeza Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa iwe taasisi inayojitegemea badala ya kuwa
sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kama ilivyokuwa katika Rasimu
ya Kwanza.
“Rasimu inapendekeza kuwepo na Jeshi moja la
polisi na Idara moja ya Usalama kwa taifa zima, siyo kama tulivyokuwa
imependekezwa katika rasimu ya kwanza kwamba kila upande unaweza
kuanzisha jeshi lake la polisi,” alisema.
Muungano
Akizungumzia Muungano na jinsi Tume ilivyofanya
uchambuzi wa pendekezo lake la Serikali tatu alisema: “Katika Rasimu ya
Kwanza tulieleza kuwa kuendelea kwa Serikali mbili kulihitaji ukarabati
mkubwa ambao tuliona hautawezekana.
“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilieleza Tume itaongozwa na
msingi mkuu wa kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha
mambo kadhaa muhimu, moja ya mambo hayo ilikuwa ni kuwapo kwa Jamhuri ya
Muungano. Tume ilianza kazi kwa madhumuni ya kupata maoni ya kuboresha
Muungano.”
Alisema watu wengi walizungumzia Muungano, lakini
wengi wao walijikita katika muundo wake. Kwa Tanzania Bara, wananchi
zaidi ya 39,000 walitoa maoni yao kuhusu muungano, kati yao 27,000
walizungumzia muundo wake. Kwa upande wa Zanzibar, kati ya wananchi
38,000 waliotoa maoni 19,000 walizungumzia muundo wa Muungano.
“Tanzania Bara asilimia 13 walitaka Serikali moja,
asilimia 24 walipendekeza Serikali mbili, asilimia 61 walipendekeza
Serikali tatu. Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza
Serikali mbili na asilimia 60 walipendekeza Muungano wa mkataba na watu
25 sawa na asilimia 0.1 walitaka Serikali moja,” alisema.
Alisema vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi
za kiraia na baadhi ya taasisi za Serikali zilipendekeza muundo wa
Serikali tatu, huku akitolea mfano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
Baraza la Katiba Ofisi ya Waziri Mkuu na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Malalamiko Muungano
Alisema kila upande wa Muungano una malalamiko
mengi kuhusu muundo na kwamba tume hiyo imeorodhesha malalamiko 10 kwa
upande wa Zanzibar na manane kwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, malalamiko matatu
makubwa ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano
ambalo linaisaidia zaidi Tanganyika kuliko Zanzibar na kuifanya
Tanganyika kuwa Tanzania.
Pili, mambo ya Muungano kuongezeka na kuathiri
madaraka na kuishusha hadhi Zanzibar na tatu ni kumuondoa Rais wa
Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema kwa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni
Zanzibar kuwa nchi huru yenye bendera yake, wimbo wa taifa, serikali
yake na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania
Bara imepoteza utambulisho wake. Katiba ya Jamhuri inasema Tanzania ni
nchi moja lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni nchi mbili.
Pili, Zanzibar imebadili Katiba yake na kuchukua
madaraka ya Jamhuri ya Muungano, kuelekeza sheria za Muungano
zinazopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe kwanza kwenye Baraza la
Wawakilishi kabla ya kutumika.
Tatu, wananchi wa Tanzania bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, wakati wenzao wana haki hiyo Tanzania bara.
Muundo wa Muungano
Alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar, Tume imebaini
kuwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano
kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania bara, hasa maendeleo na uchumi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977,
Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano na
yasiyo na muungano kwa upande wa bara... “Kwa msingi huo, Serikali ya
Muungano inashughulikia sana kilimo, elimu, afya, maji, nishati na
madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania
bara yasiyo ya Muungano.”
Alisema kutokana na hali hiyo, Tume haikuwa na
njia nyingine kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka ya kutosha
juu ya mambo ya maendeleo na uchumi kwa upande wa Zanzibar na kwamba
hata utafutaji wa rasilimali zaidi ni kwa ajili ya Tanzania bara kuliko
Zanzibar.
Alisema Zanzibar inafanya mipango yake ya
maendeleo, kwamba ili ipate rasilimali, kama mikopo na misaada, ni
lazima ipitie Serikali ya Muungano jambo ambalo utekelezaji wake
umesababisha matatizo mengi.
“Njia pekee ambayo ingeiwezesha Zanzibar kufaidi
shughuli za Serikali ya Muungano wa maendeleo ya Zanzibar ni mambo yote
kuwa chini ya Muungano kwa maana ya kuwa na Serikali moja, lakini hilo
likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa,” alisema.
Alisema tume hiyo imefanya uchambuzi wa mambo 22
ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi ya uhuru wa Zanzibar na
kubaini kuwa siyo yote yanayotekelezeka. Mengi yamebadilishwa bila
kubadili Katiba au kwa makubaliano ya pande mbili.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kodi, bandari,
viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, posta na simu, uraia,
takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufaa.
“Kama Katiba ya Zanzibar ikibaki kutakuwa na nchi
mbili; zikiwa nchi mbili haitawezekana nchi moja iwe na hadhi na uhuru
na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru, kwa tathmini yetu, tunaona
ukarabati huu ni mgumu. Serikali tatu ndiyo suluhisho,” alisema.