Dar es Salaam. Unaweza kusema sasa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula
kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015
watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
“Wapo watu wanataka waichanechane CCM kwa sababu
ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata urais. Kuna
makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe hatuwezi
kuyafumbia macho.”
Akifafanua hilo Mangula alisema: “Tutawaita wote
walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini wanafanya
hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza katika mikutano
wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu,
tunajua dhamira yao ni nini.”
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja
tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kusema
mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda
mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya Lowassa siku mbili
zilizopita, kutangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari
aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za
Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa
wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,
alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya,
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa
Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama hicho
wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya
Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu
za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa kusoma
kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi mambo
mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa CCM na
wanachama taifa, Masoud Mbengula.
Moja ya kanuni hizo inasema “Ni mwiko kwa kiongozi
wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au eneo
analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye
mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono.”
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za chama
hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa msaliti na
hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama wakati
wowote.
“Tutawachukulia hatua kali wale wote ambao wameanza kuonyesha
dalili kama hizo za kutoa michango, misaada, zawadi. Lengo la mwanachama
huyo ni kutaka kuungwa mkono, wanaotaka madaraka wasubiri muda ufike
ndiyo wafanye hivyo.”
Aliongeza “Hivi haya mapenzi ya kusaidia yameanza
lini, fedha hizo zinatoka wapi, hawa wanaosadiwa wanatakiwa kutambua
kuwa yote hayo ni kampeni kwa kuwekeza, hatuwezi kuwa na viongozi wa
nchi wa namna hii wa uchu wa madaraka, CCM haitawafumbia macho lazima
kanuni na miongozo ifuatwe.”
“Kuna watu wameanza kudhani kuwa muda wa kampeni
umeanza, muda wa kampeni haujafika na hakuna majina yaliyotangazwa ya
kugombea udiwani, ubunge hata urais,” alisema Mangula na kuongeza;
“Kuna makundi yanaifanya nchi ya Somalia
isitawalike. Makundi ya aina hiyo naona yapo hata CCM; watu wanaibua
vita ya maneno ndani ya chama, wanataka wakichanechane chama kwa sababu
ya uroho wa madaraka tu.”
Bila kuyataja makundi hayo Mangula alisema:
“Utaongozaje nchi ambayo imegawanyika katika makundi? Watu wameanza
kuvuruga chama chetu, kila mtu ana kundi lake na wakati mwingine
wanayatumia makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia
macho hata kidogo.”
Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Makamba hivi karibuni amekuwa akitoa misaada kwa
vikundi vya waendesha bodaboda katika mikoa mbalimbali, hali ambayo
inatafsiriwa kuwa ni kujiimarisha kisiasa.
Hata hivyo, mwaka jana Rais Jakaya Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa alinukuliwa akisema kuwa sio vibaya kwa
wanachama wa chama hicho kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi
ndani ya chama, lakini siyo kufanya kampeni.
Mei 26 mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama kitamwadhibu bila
huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo mbalimbali na
kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.
Akifunga mafunzo ya makatibu na wenyeviti wa
wilaya na mikoa mjini Dodoma mwaka jana, Rais Kikwete alisema kuwa
inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha
kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili
wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama bunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao
wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za
kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia
hadhi chama hicho.
Uchaguzi Serikali za Mitaa
Mangula akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika
mwaka huu alisema, viongozi wote wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni
na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
“Vitendo vya rushwa ndio vilitufanya katika
chaguzi zilizopita kufanya vibaya, watu walinunuliwa kadi, sasa viongozi
wa matawi wawe makini tusirudi tulikotoka na tukibaini mtu hafuati
kanuni tutamwajibisha,” alisema Mangula.
Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua. Ut enim ad minim veniam, quis nostrud exercitation.
0 comments:
Post a Comment